Saturday, July 4, 2009

Watu hupata viongozi wanaowastahili

1.
Huanza na tonge kubwa, Akiwa yu mwanafunzi,
Ugali au ubwabwa, Kadhalika na mchuzi,
Nyumbani kwao hubebwa, Wazazi yao mapenzi,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

2.
Mtazame bado mdogo, hutamani kila kitu,
Chipsi hata muhogo, hata vikiwa vya watu,
Wazazi kwao mikogo, 'Kajanjaruka mwenetu'
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

3.
Adabu kapewa kisogo, tunalea mbwa mwitu,
Sasa madubu na mbogo, hakika kizazi chetu,
Ususi na mikorogo, ndio Uafrika wetu,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

4.
Kuitwa manyani haki, tumezidi mno kuiga,
Weusi hautambuliki, asili twaizugazunga,
Waupe hatuthaminiki, watushangaa maboga,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

5.
Shuleni ni mshindani, tena kwa shari si heri,
Mtu wa misheni tauni, Muislamu si kafiri,
Na hakosi kanisani, Jumapili alfajiri,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

6.
Chuoni akiingia, rushwa keshagundua,
Ofisini huanzia, darasani kuishia,
Walimu wanamjua, yawaponza yao njaa,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

7.
Maksi zake bandia, hakuna lililoingia,
Akilini kumkaa, masomo kanyanyapaa,
Njia mkato hutumia, ujinga yake silaha,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

8.
Wengine chupi huvua, gredi wakapatiwa,
Madaktari hujakua, na heshima wakapewa,
Ila moyoni wanajua, maisha yao kinyaa,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

9.
Hujiunga na siasa, kwa binafsi manufaa,
Si wananchi ni anasa, anayoitumikia,
Kumbe kisa na mkasa, mwana baa na balaa,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

10.
Uchaguzi kiingia, nao pia hugombea,
Wakazaini majuha, mwishowe kuwachagua,
Wakijua yao njaa, sasa itajapotea,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

11.
Ukiwapa kura tambua, kula umewapatia,
Tena hawatokutambua, hukithiri yao njaa,
Matonge hujimegea, ikesha taifa sinia,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

12.
Hakuna kinachobakia, bali njaa na ukiwa,
Ndoto zote hung'olewa, jinamizi kuingia,
Ndio tuliowachagua, hisani watugawia,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

No comments: