Monday, January 9, 2012

Huenda nje wasirudi na lolote jipya....

VIGOGO na Vizito nchini wanajua kinachotokea wanapoingia kwenye ndege kwenda majuu au kurudi nyumbani. Maisha ya kwenye ndege hufanana na yale ya huko nje kunakoitwa kuliko endelea.

Kwa bahati nzuri au mbaya wakubwa wanaporudi Tanzania hupokewa na magari yao yenye viyoyozi na kupelekwa kwenye majumba yao ya kifahari au ofisi zao zenye viyoyozi wakaendelea na starehe nyumbani kama waliyokuwa nayo kwenye ndege na huko ugenini.

Mswahili wa Kariakoo, hata hivvyo, anayelazimika kupanda daladala uwanja wa ndege kurudi nyumbani huona ghafla karudia kwenye jalala lile lile alilotoka.

Jambo hili, lipo, linaendelea na hakuna kiongozi ambaye kwa mamia ya safari zake nchi za nje ameshawahi kuinufaisha nchi na wananchi wakawa na hali nafuu zaidi ya ile waliyokuwa nayo kabla ya safari zake.

Huondoka, wakenda, wakarudi na kichwani hakuna kitu (sifuri kabisa) kuhusiana na kuinua miji na nchi yao ikafanana fanana anagalau na kule wanakotoka. Bila shuka wanapofika huko hufunga macho na masikio yao na wakaishiwa kudanganywa kwa hili na lile, kama sio kukubali kuwa Mwafrika kamwe hawezi kuwa na maisha kama ya mzungu chini ya uongozi kama wao.

Hoteli za Kiswahili na utu wa mzawa...

SERA za kitalii zinazohakikisha kwamba hoteli ya kitalii ina vyoo na maliwato zenye tailzi, zinazonukia vizuri na safi wakati wote lakini zinashindwa kuchangia mabadiliko ya hoteli za Kiswahili ingawa zikawa na huduma ya vyoo safi sio sera zinazojali uhai na ubora wa maisha ya mzawa na mwananchi.

Ni sera za seramala kukalia maboksi au magogo au la mfinyanzi kuacha mkewe akipikia vigae. Na viongozi wasio na habari kwa kinachotokea kwa mamilioni ya watu wao, lakini wakawa wanataka kujua kila kitu kinachowatokea wazungu kumi au mia waliopo nchini sio viongozi wanaoweza kuipeleka nchi popote pale pa kujivunia.

Rasilimali asili na wazawa ni bora kuliko wawekezaji na mitaji toka nje.....

NADHARIA zinazozaliwa nyumbani badala ya kutoka ugenini, aghalabu, kwa wakoloni zinatoa umuhimu wa juu kabisa katika kuwathamini wazawa kama rasilimali endelevu na ya kudumu kwa maendeleo ya nchi inayokusudia kuwa huru kikwelikweli.

Nadharia hii inatoa kipaumbele kwa rasilimali nyumbani zaidi kuliko rasilimali azimishi. Mantiki ikiwa cha nje huweza kuondolewa wakati wowote, lakini cha ndani hakiwezi kuondolewa chote.

Sera zinazofuatwa na serikali kama ile ya Tanzania ni za kizamani na zenye mashiko yake toka kwenye ukoloni na haziwezi kamwe kuwa chachu ya maendeleo ya nchi hiyo.

Sera hizi ni zile zinazolazimisha kumpa mtu mshahara mkubwa tu eti kwa sababu ni mwanasiasa au mtumishi wa serikali bila kuoanisha mchango wa mhusika na maendeleo yanayoonekana na kukubalika katika eneo husika.

Halafu kama vile kwa kuambizana serikali nyingi za Kiafrika kwa umasikini wao wa mawazo zimeridhia daktari alipwe mshahara mdogo kuliko mbunge asiyesoma kabisa; mwalimu alipwe ujira mdogo kuliko mkuu wa mkoa au wilaya anayevuruga na kurudisha nyuma eneo analotakiwa kuendeleza; au nesi kulipwa mshahara mdogo kuliko kiongozi wa kuteuliwa ambaye huishia kufanya mengi kwa manufaa yake binafsi na jamaa zake na siyo ya wananchi.

Nadharia ya kileo katika masuala ya kuthamini na kuheshimu zaidi rasilimali yetu wenyewe ina mapendekezo mbalimbali ya kuondokana na udhalimu huu wa miaka kadhaa. Mojawapo kubwa likiwa ni kwa wabunge katika mabunge na mabaraza yetu kulipwa mshahara kulingana na elimu na ujuzi walio nao na sio vinginevyo.

Aidha, watumishi wanaochangia waziwazi kuokoa maisha ya watu; kubadilili maisha na mwelekeo wa watu na nchi; na wote wanaoutmia nguvu au musuli zao, akili au maarfia yao, uwezo au vipaji vyao watakuwa wakipata mishahara mikubwa pengine kuliko wabunge na mawaziri. Na hivyo kuondoa uroho wa watu kukimbilia kuwa wabunge au mawaziri wakati uwezo hawana kwa sababu ya tamaa ya cheo na fedha tu.

Thursday, September 16, 2010

Nyani achekapo Kundule

Kwa asilimia 99 ya Watu weusi duniani na hususan Waafrika hakuna anayeweza kumcheka mwenzie katika masuala ya ngono na uzinzi. Tumekubuhu, Ukiona kuna wanaocheka basi wamithiishe na nyani achekaye kundu la mwenzie !

Uafrika hausimami bila ya mambo kama hayo. Vinginevyo huyo Mwafrika bandia. Jamani tuambieni ukweli kwani Der Spiegel llishafanya utafiti wenye mizizi toka kwa Sigmund Freud na tunayoona katika mizunguko yetu ya kila siku hapa hapa nchini.


Njia muafaka ni kukubali kuwa sisi sote tuko kama tulivyo na ndivyo tulivyoumbwa na kazi ianze kuoanisha maumbile yetu na kile kinachotakiwa. Maana ngono haizui kuwa na taifa imara kiuchumi na madhubuti katika ustawi wa jamii. Inawezekana kuchanganya raha zetu na karaha zetu, utamu na uchungu wetu, ubaya na uzuri wetu kisha tukapata kilicho bora na chenye baraka zaidi.

Saturday, July 4, 2009

Watu hupata viongozi wanaowastahili

1.
Huanza na tonge kubwa, Akiwa yu mwanafunzi,
Ugali au ubwabwa, Kadhalika na mchuzi,
Nyumbani kwao hubebwa, Wazazi yao mapenzi,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

2.
Mtazame bado mdogo, hutamani kila kitu,
Chipsi hata muhogo, hata vikiwa vya watu,
Wazazi kwao mikogo, 'Kajanjaruka mwenetu'
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

3.
Adabu kapewa kisogo, tunalea mbwa mwitu,
Sasa madubu na mbogo, hakika kizazi chetu,
Ususi na mikorogo, ndio Uafrika wetu,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

4.
Kuitwa manyani haki, tumezidi mno kuiga,
Weusi hautambuliki, asili twaizugazunga,
Waupe hatuthaminiki, watushangaa maboga,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

5.
Shuleni ni mshindani, tena kwa shari si heri,
Mtu wa misheni tauni, Muislamu si kafiri,
Na hakosi kanisani, Jumapili alfajiri,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

6.
Chuoni akiingia, rushwa keshagundua,
Ofisini huanzia, darasani kuishia,
Walimu wanamjua, yawaponza yao njaa,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

7.
Maksi zake bandia, hakuna lililoingia,
Akilini kumkaa, masomo kanyanyapaa,
Njia mkato hutumia, ujinga yake silaha,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

8.
Wengine chupi huvua, gredi wakapatiwa,
Madaktari hujakua, na heshima wakapewa,
Ila moyoni wanajua, maisha yao kinyaa,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

9.
Hujiunga na siasa, kwa binafsi manufaa,
Si wananchi ni anasa, anayoitumikia,
Kumbe kisa na mkasa, mwana baa na balaa,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

10.
Uchaguzi kiingia, nao pia hugombea,
Wakazaini majuha, mwishowe kuwachagua,
Wakijua yao njaa, sasa itajapotea,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

11.
Ukiwapa kura tambua, kula umewapatia,
Tena hawatokutambua, hukithiri yao njaa,
Matonge hujimegea, ikesha taifa sinia,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

12.
Hakuna kinachobakia, bali njaa na ukiwa,
Ndoto zote hung'olewa, jinamizi kuingia,
Ndio tuliowachagua, hisani watugawia,
Akija kuwa kiongozi na wote atabebwa.

Friday, March 13, 2009

uchumi arijojo

Waliokopa kwa fujo,
na wakopeshaji chizi,
Wametuletea rojo
Uchumi arijojo!

Wamekalia porojo,
Baada ya fumanizi,
Sasa twapata maonjo
Uchumi arijojo!

Hawataki baya tajo,
Waogopa masimulizi,
Wazidi kukaa chonjo
Uchumi arijojo.

Viongozi wetu bojo,
Jengine hawaliwezi,
Hawajaingia dojo
Uchumi arijojo!

Yataka kubwa mchujo,
Kuiepuka wachuuzi
Wa choo hata mikojo
Uchumi arijojo!

Wahindi wana matejo,
Waarabu Abunuwazi,
Wachina nao mapunjo
Uchumi arijojo!

Tiara arijojo,
Yalazimu mageuzi,
Visheni matarajio
Azma ni mategemeo!

Uchumi arijojo,
Hauivi utegemezi,
Kamuulize Ndesanjo,
Kule Hai au Vunjo!