Monday, January 9, 2012

Huenda nje wasirudi na lolote jipya....

VIGOGO na Vizito nchini wanajua kinachotokea wanapoingia kwenye ndege kwenda majuu au kurudi nyumbani. Maisha ya kwenye ndege hufanana na yale ya huko nje kunakoitwa kuliko endelea.

Kwa bahati nzuri au mbaya wakubwa wanaporudi Tanzania hupokewa na magari yao yenye viyoyozi na kupelekwa kwenye majumba yao ya kifahari au ofisi zao zenye viyoyozi wakaendelea na starehe nyumbani kama waliyokuwa nayo kwenye ndege na huko ugenini.

Mswahili wa Kariakoo, hata hivvyo, anayelazimika kupanda daladala uwanja wa ndege kurudi nyumbani huona ghafla karudia kwenye jalala lile lile alilotoka.

Jambo hili, lipo, linaendelea na hakuna kiongozi ambaye kwa mamia ya safari zake nchi za nje ameshawahi kuinufaisha nchi na wananchi wakawa na hali nafuu zaidi ya ile waliyokuwa nayo kabla ya safari zake.

Huondoka, wakenda, wakarudi na kichwani hakuna kitu (sifuri kabisa) kuhusiana na kuinua miji na nchi yao ikafanana fanana anagalau na kule wanakotoka. Bila shuka wanapofika huko hufunga macho na masikio yao na wakaishiwa kudanganywa kwa hili na lile, kama sio kukubali kuwa Mwafrika kamwe hawezi kuwa na maisha kama ya mzungu chini ya uongozi kama wao.

No comments: